MBEYA City Council FC imeutumia vizuri Uwanja wa nyumbani, Sokoine mjini
Mbeya baada ya kuwafunga mabingwa watetezi, Yanga mabao 2-1.
Ushindi huo wa kwaza kwa Mbeya dhidi ya Yanga tangu wapande Ligi Kuu,
unaifanya MCC ifikishe pointi 19 baada ya kucheza mechi 14, wakati Yanga
inabaki na pointi zake 27 za mechi 13.
Mbeya City waliuanza vizuri mchezo na kufanikiwa kumaliza kipindi cha kwanza wanaongoza kwa mabao 2-1.
Beki wa kushoto wa MCC, Hassan Mwasapili aliifungia timu yake bao la
kwanza dakika ya sita baada ya kumtungua vizuri kipa wa Yanga, Deo
Munishi ‘Dida’ kwa shuti la mbali la mpira wa adhabu.
Nahodha Kenny Ally akaifungia Mbeya City bao la pili dakika ya 36 kwa
shuti la mbali pia baada ya kuanzishiwa mpira wa adhabu na beki wa kulia
Haruna Shamte, aliyechezewa rafu na beki wa Yanga, Hassan Kessy.
Bao hilo lilizua utata baada ya wachezaji wa Yanga kumfuata refa Rajab
Mrope wa Ruvuma kulikubali, kulikataa baada ya kuzongwa na wachezaji na
Yanga na kulikubali tena baada ya majadiliano na wasaidizi wake.
Lakini kilichoonekana ni wachezaji wa Yanga walikuwa wamezubaa
hawakujipanga na Shamte akatumia mwanya huo kumuanzishia mfungaji
haraka, ambaye aliunganishia shuti nyavuni.
Wachezaji wa Mbeya City wakamvamia refa huyo na wakati huo huo mashabiki
wao waliingia uwanjani na wengine walikuwa wakirusha chupa za maji
kutoka jukwaani, hadi amani ikachafuka uwanjani.
Wakati huo huo refa huyo alikuwa akizongwa na wachezaji wa Mbeya City na
ghafla akageuka na kulibariki hilo, hivyo mchezo kuendelea.
Mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma akaifungia Yanga bao la kwanza
dakika ya 45 baada ya kuwatoka mabeki wa Mbeya City na kumtungua kipa
Mmalawi Owen Chaima.
Kipindi cha pili, kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm alianza
kumpumzisha kiungo wa ulinzi, Mbuyu Twite na kumuingiza Mzimbabwe,
Thabani Kamusoko kabla ya baadaye kumtoa winga Deus Kaseke na kumuingiza
Geoffrey Mwashiuya.
Katika kipindi hicho cha pili, Kocha Mmalawi wa Mbeya City alionekana
kubadilisha mbinu na kuamua kucheza mchezo wa kujihami kuulinda ushindi
wao, hivyo kuwapa kazi Yanga ya kuupasua ukuta wao.
Kinara wa mabao wa Yanga, Amissi Joselyn Tambwe hakuwa katika siku nzuri
leo baada ya kukosa bao wazi dakika ya 64 akiunganishia nje kwa kichwa
krosi ya Ngoma.
Mbeya City waliendelea kucheza kwa kujihami hukui wakipeleka
mashambulizi ya kushitukiza langoni mwa Yanga hadi kipyenga cha mwisho.
Wachezaji wa Yanga wakamvaa tena refa wakidai amemaliza mchezo kabla ya
muda, hivyo kusababisha atolewe uwanjani kwa msaada wa Jeshi la Polisi.
Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Owen Chaima, Haruna Shamte, Hassan
Mwasapili, Sankhani Mkandawile, Rajab Zahir, Tumba Lui, Raphael Daud,
Kenny Ally, Ditram Nchimbi, Hamedy Murutabose/Omary Ramadhani dk18 na
Joseph Mahundi/Issa Nelson dk90+.
Yanga; Deo Munishi ‘Dida’, Hassan Kessy, Mwinyi Haji Mngwali, Andrew
Vincent, Vincent Bossou, Mbuyu Twite/Thabani Kamusoko dk46, Simon Msuva,
Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe/Obrey Chirwa dk68, Donald Ngoma na Deus
Kaseke/Geoffrey Mwashiuya dk51